HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPIGA HATUA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI.

Na Mwandishi Wetu,
Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma

Serikali imesema imepiga hatua kubwa katika kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini kwa kutelekeza programu mbalimbali za utoaji elimu na huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma akitoa taarifa ya mafanikio ya Ofisi yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.



Mhe. Pindi amesema miongoni mwa hatua kubwa zilizopigwa na serikali ni pamoja na kudhibiti vifo vitokanavyo na UKIMWI ambapo vimepungua kwa asilimia 50 kutoka 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2021.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja mafanikio ya Serikali yaliyoshuhudiwa katika eneo hili ni kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya ya VVU katika jamii ikiwemo maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kushuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2021,”alisema Mhe. Pindi.

Akibainisha mafanikio mengine katika mapambano dhidi ya UKIMWI alisema kwamba ni kushuka kwa kiwango cha unyanyapaa katika jamii kutoka asilimia 28 mwaka 2013 hadi asilimia 5.5 mwaka 2021, na Nchi kuwa katika hatua nzuri za kufikia malengo ya Kidunia ya Tisini Tatu (90-90-90) mwaka 2020 na Tisini na Tano Tatu (95-95-95) mwaka 2025.

“Wanaofahamu hali zao za mambukizi ni asilimia 83, wanaofahamu hali zao za mambukizi na wapo kwenye matibabu ni asilimia 98 na waliopo kwenye matibabu na wamefubaza VVU ni asilimia 92,”alieleza Waziri Pindi.

Kuhusu Ujenzi

Pia akitaja mafanikio mengine ya Serikali ya Awamu ya Sita alifafanua kuwa ni pamoja na Uzinduzi wa ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali ambao unaendelea na ukitarajiwa kukamilika mwaka 2022/23.

“Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara zenye urefu wa KM 51.2 katika mji huo zinajengwa kwa kiwango cha lami. Katika mwaka 2021/22 jumla ya Shilingi bilioni 300 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi na Miundombinu,”Alibainisha.

Mh.Waziri Pindi Chana akifanya Uzinduzi wa ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali ambao unaendelea na ukitarajiwa kukamilika mwaka 2022/23.


Kuhusu mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya Mhe. Pindi alisema Kliniki sita za tiba ya Methadone zimeanzishwa katika mikoa ya Songwe,Arusha na zingine nne Jijini Dar es Salaam hivyo kufanya kliniki hizo kufikia 15 Nchi nzima zinazohudumia zaidi ya waathirika 10,600 wa dawa za Kulevya kila siku.

“Serikali imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya Methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa Heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake na ili kuhakikisha wanainuka kiuchumi vijana 200 wanaopatiwa matibabu kwenye kliniki za Methadone wamejumuishwa katika Programu ya Kukuza Ujuzi kupitia Vyuo vya VETA ili kuwajengea ujuzi wa kufanya kazi za kiuchumi,” Alifafanua Mhe. Pindi.

Aidha alieleza kwamba Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa njia mbalimbali ambapo vilabu vya kupinga dawa za kulevya vimeanzishwa shuleni na walimu 66 wamepatiwa elimu ili kuwawezesha kusimamia klabu hizo, vyuoni na elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya ambapo inakadiliwa zaidi ya wananchi millioni 10 wamefikiwa na elimu hiyo.

“Serikali imeendelea kuhakikisha inadhibiti matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kuwanusuru wananchi wake kuathirika na dawa hizi kwahiyo hatua hii ya Serikali imesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia wimbi la vijana kuingia kwenye matumizi na biashara ya dawa hizo,”


Post a Comment

0 Comments