HEADLINES

6/recent/ticker-posts

MBOLEA ZA RUZUKU KUONGEZA USALAMA WA CHAKULA NCHINI


Na Mwandishi Wetu,

Songwe,

Mkuu wa mkoa wa Songwe, Waziri Waziri Kindamba amesema mbolea za ruzuku zinazotolewa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa msimu wa kilimo 2022/2023 zimelenga kuhakikisha kuna usalama wa chakula nchini.

“Usalama wa chakula ni usalama mkubwa kuliko usalama mwingine wowote duniani  ili kuwa na amani ni lazima suala la usalama wa chakula lipewe kipaumbele”, Kindamba alisisitiza.

Mkuu wa Mkoa Kindamba ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Oktoba, 2022 wakati akifungua maadhimisho ya siku ya mbolea duniani yenye kauli mbiu “ *Agenda10/30: Matumizi sahihi ya Mbolea ya Ruzuku kwa Kilimo chenye Tija”* yanayofanyika kitaifa mkoani Songwe yakiambatana na maonesho kutoka kampuni mbalimbali za mbolea pamoja na taasisi zilizopo kwenye mnyororo wa chakula nchini.

Amesema, kauli mbiu hiyo imelenga kuonesha dhamira ya Serikali ya Rais Samia katika kuthamini mchango wa Sekta ya Kilimo na kuamua kutenga kiasi cha shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku za mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei za mbolea na kuwawezesha kulima kilimo biashara.

Akizungumzia kauli mbiu hiyo kwa upande wa wakulima, kindambwa amesema, inawahamasisha wakulima wakubwa kwa wadogo nchini kutumia mbolea katika uzalishaji wa mazao ili kuweza kuzalisha mazao mengi katika eneo dogo.

 Kindambwa aliongeza kuwa, ili kuwa na uzalishaji wenye tija ni vyema wakulima wapewe elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kuelimishwa juu ya afya ya udongo ili wanapotumia mbolea za ruzuku wapate matokea chanya na kuongeza usalama wa chakula nchini.

Akizungumzia juu ya utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi wa  asilimia 90 Kindambwa aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhamasisha uwekezaji wa ndani ili kuwe na uwiano wambolea inayozalishwa nchini kwa asilimia 50 na asilimia 50 kwa zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili pesa ya serikali inayotolewa kwa ajili ya ruzuku iwanufaishe wazawa na wawekezaji wa mbolea waliopo ndani ya nchi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kindambwa ameishauri TFRA kupeleka wawekezaji wa viwanda vya mbolea katika mikoa inayojihusisha zaidi na kilimo hususani mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambako matumizi ya mbolea yapo juu ili bidhaa hiyo iwafikie wakulima kwa wakati na kwa bei himilivu.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Songwe, Eliniko Mkola amesema Ilani ya chama Cha Mapinduzi kipengele cha 3 inaelekeza kuongeza uzalishaji wa mazao na kuongeza usalama wa chakula nchini na ndio maana serikali imeamua kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku.

Pia, Mkola ameyataka  makampuni yaliyopewa kazi ya kusambaza mbolea za ruzuku nchini kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia wakulima katika maeneo wanakofanyia shughuli za kilimo ili azma ya serikali ya kutenga bajeti kwa ajili ya ruzuku iweze kufikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo bei elekezi ya mbolea kwa mkulima yeyote nchini ni  shilingi elfi 70.

Dkt. Ngailo amefafanua kuwa kwa maeneo ambayo gharama za usafiri ili kufikisha bidhaa hiyo kwa wakulima imekuwa kubwa, kamati za pembejeo za wilaya ziwasilishe maoni ya kiasi kinachozidi ili kuweza kufidiwa kupitia fedha iliyotengwa kwa ajili ya ruzuku.

Mwisho, Dkt. Ngailo ametoa wito kwa wakulima  kujisajili kwa wakati ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku pindi msimu unapoanza na si kuanza kujisajili wakati wa msimu kwani hawatapata matokeo wanayotarajia kutokana na kutokufuata kanuni bora za kilimo.

Amesema kanuni bora za kilimo zinazomtaka mkulima kuandaa shamba kwa wakati, kupanda kwa mbolea, kupalilia na kukuzia  kwa kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea na kwa wakati.



Post a Comment

0 Comments