HEADLINES

6/recent/ticker-posts

MADEREVA WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI ILI KUEPUKA AJALI ZA BARABARANI



Na. Catherine Sungura, Tabora

Wananchi pamoja na madereva wanaoendesha vyombo vya moto nchini wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari wanapokua wanatumia barabara kwa kufuata sheria za barabarani kuepusha ajali kwa wao wenyewe au watumiaji wa barabara ili kupunguza ajali na kuepushia Serikali kutumia gharama kubwa za kuwahudumia wagonjwa wanaotokana na ajali za hizo.

Rai hiyo imetolewa leo na  Dakatari Bingwa wa Mifupa na Majeruhi  kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda- Kamanga ya  jijini Mwanza  Dkt. Fikiri Martin wakati wa kambi ya utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa wa Tabora inayofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete.

“Niwahimize wananchi wachukue tahadhari wanapotumia barabara kwa kufuata alama, sheria za barabarani na kwa wale wanaotumia vyombo vya moto  kuwa na leseni  na kuzihuisha leseni zao pia kuendesha vyombo hivyo wakiwa wanajihami ili kuepusha ajali kwa wao wenyewe au kwa watumiaji wengine wa barabara”.

Ameongeza kuwa ni  vyema kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto kujenga mazoea ya kufunga  mikanda  na kwa madereva kuendesha magari kwa mwendo unaoendana na hali ya  barabara.


Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani Dkt. Adam Gembe wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani-Tumbi amewasisitiza wagonjwa wa Moyo,Kisukari  kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kulingana na maelekezo ya wataalam wa afya.

Kwa upande wa madereva wa bodaboda Dkt. Martin amesema ni vyema waendelee kuvaa kofia ngumu na kuzingatia suala zima la mwendo pamoja na kuwajali abiria wao na wanaowapita barabarani.

“Boda boda ni ajira kubwa na tutaendelea kuwatumia hivyo ni vyema wakawa makini, wakaweka kipaumbele cha afya zao mbele  kwani endapo atapata ajali na kuumia mguu au vinginevyo unakua na  asilimia hamsini ukapona kabisa au ukatibiwa na kubaki na madhara maisha yako yote, kimsingi ni kuendesha kwa kufuata sheria za barabarani na kuweka maisha yako salama.

Kuhusu kambi hiyo  ya utoaji wa huduma za kibingwa  Dkt. Martin amewashukuru wananchi ambao wamejitokeza kupata huduma za kibingwa  na zaidi ya wagonjwa wa mifupa mia mbili na hamsini  wameonwa katika idara hiyo na baadhi ya wagonjwa waliopata ajali hivi karibuni wamefanyiwa upasuaji wa kuwekewa vyuma kwa ajili ya kuunga mifupa ipate muelekeo wake wa zamani.

Naye, mmoja wa wazazi waliopatiwa huduma za kibingwa idara ya mifupa  katika kambi hiyo Bi. Helena Salumu anayeishi kata ya Kiloleni ameishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma hizo katika hospitali ya Kitete na kutoa ushauri kwa wazazi wengine kutokukata tamaa kwani huduma zipo na hivyo kuwapeleka watoto wao  kwenye vituo vya kutolea huduma pale wanapoona  matatizo na kuongeza kuwa mwanaye huyo mwenye umri wa miaka minne aliyapata matege hayo akiwa ameanza kutembea na kwamba mtoto wake alipokuwa akisimama.

Post a Comment

0 Comments