HEADLINES

6/recent/ticker-posts

DK. KOMBA AHIMIZA WAZAZI KULINDA MAADILI YA WATOTO VYUONI


Na Mwandishi Wetu,

DAR ES SALAAM,

WAZAZI nchini ambao watoto wao wamehitimu kidato cha sita kwa mwaka 2023 wametakiwa kuhakikisha wanaendelea kuweka uangalizi kwa watoto wao katika maadili wanapoelekea kwenye masomo ya Vyuo vikuu.

Wito huo umetolewa jana tarehe 20/5/2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk.Aneth Komba katika mahafali ya 22 ya Kidato cha Sita ya shule ya Sekondari ya Loyola ya Mabibo jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa, Wanafunzi hao wanapaswa kuendelea kuangaliwa hasa kwenye masuala ya malezi ili waweze kufikia malengo yao ya maisha.

"Wazazi kazi yetu ya kulea haijaishia hapa, tuendelee kuwafuatilia watoto wetu ili waendelee kusoma na kufikia malengo yao "amesema Dk.Komba.

Aidha, Akijibu hotuba iliyotolewa na Mkuu wa shule ya Loyola, Padri  Martin Wawelu  kuhusiana na rasimu za Sera na Mitaala, Dk.Komba ameeleza kuwa maoni yote ameyapokea na kuwa yatafikishwa katika maboresho ya rasimu hizo na kueleza kuwa maoni yanaendelea kutolewa na kupokelewa hadi tarehe 31/5/2023.

Naye Mkuu wa shule, Padri Wawelu ameipongeza Serikali kwa maboresho mbalimbali ya Elimu yenye kuleta tija nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk.Aneth Komba akitoa Cheti kwa mmoja ya wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Loyola

Katika mahafali hayo,TET imetoa zawadi ya vitabu vya kiada  nakala 60  kwa shule ya Loyola zenye thamani ya shilingi 865,000 ambapo Mkurugenzi Mkuu amewaomba uongozi wa shule hiyo kuwapa nafasi wanafunzi wote kuweza kupata muda wa kusoma vitabu hivyo ambavyo vitawekwa kwenye maktaba za shule hiyo.

Mahafali hayo Wanafunzi 89 kati yao Wavulana 53 na Wasichana 36 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 15 zaidi ya wahitimu wa mwaka jana,2022.

Wanafunzi hao wanafikisha jumla ya Wanafunzi 7,319 waliohitimu toka mahafali ya kwanza shuleni hapo mwaka 1999.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule zaidi ya 845 duniani kote zinazoongozwa na Shirika la Yesu, Shirika la Mapadre wa Kanisa Katoliki (yaani Society of Jesus wanaojulikaja kama JESUITS).

Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk.Aneth Komba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa kidato cha Sita shule ya Sekondari ya Loyola ya Mabibo jijini Dar es Salaam mwaka 2023,

Post a Comment

0 Comments