HEADLINES

6/recent/ticker-posts

TANTRADE NA UCSAF WASHIRIKIANA KUTOA HUDUMA YA INTERNET MAONESHO YA SABASABA

 

Na mwandishi wetu,

DAR ES SALAAM,

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) pamoja na Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote( UCSAF)  wamekutana na kufanya kikao cha jinsi ya kutoa huduma ya mawasiliano ya interneti  WiFi (Wireless Internet) kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K Nyerere kwa kipindi chote cha  Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (almaarufu Maonesho ya SabaSaba) yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni - 13 Julai, 2023. 

Kikao hicho kimefanyika tarehe 08 Juni 2023,  katika Ofisi za TanTrade Dar es Salaaam kwa lengo la  kuboresha na kurahisisha miundombinu ya  mawasiliano ili  kuwasaidia washiriki pamoja na watembeleaji kuweza kupata mawasiliano kwa njia rahisi na haraka zaidi  katika kipindi chote cha Maonesho hayo.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Fortunatus Mhambe, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara, TanTrade kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bi. Latifa M. Khamis  ameishukuru  Taasisi  ya UCSAF kwa kutoa huduma hiyo inayolenga kurahisisha mawasiliano na kuboresha Maonesho  yawe na mvuto zaidi.

‘Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, natoa shukrani zangu za dhati kwa Taasisi  ya UCSAF kwa  kukubali kuboresha huduma za internet katika kipindi cha Maonesho, hivyo tunapenda kuuhabarisha Umma kwamba katika Maonesho hayo, huduma za Internet zitakuwa zimeimarishwa na kuboreshwa kwa ajili ya watembeleaji na waoneshaji na kuwarahisishia kuonesha biashara zao kwa njia rahisi zaidi’ alisema.

Naye Mratibu kutoka UCSAF - Kanda ya Pwani Bw. Baraka Elieza amesema kuwa Taasisi ya UCSAF itahakikisha kuwa huduma za Internet zinakuwa nzuri na zenye kuleta tija katika Uwanja wa Maonesho na kuwafanya waoneshaji pamoja watembeleaji kuweza kufurahia huduma hizo kuanzia tarehe 28 Juni - 13 Julai, 2023.

Post a Comment

0 Comments