HEADLINES

6/recent/ticker-posts

WANANCHI KUTOKA NGORONGORO WAENDELEA KUMIMINIKA MSOMERA

 


Na Mwandishi Wetu,
ARUSHA.

Hamasa ya kujiandikisha na kuhama kwa hiari  kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni inazidi kupamba moto baada ya kundi la 5  la awamu ya pili kuhama likiwa  na kaya 67 zenye watu 592 na Mifugo 2,790.

Wananchi hao waliokuwa wakiishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuamua kuhama kwa hiyari wameagwa rasmi siku ya Alhamisi  01.02.2024  na Kamishina wa Uhifadhi  wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  Bw.Richard Kiiza ambapo  aliwaomba wenyeji wanaohama kutumia fursa waliopata kuendelea kuwapa habari na kuwashawishi ndugu zao ambao bado hawajajiandikisha ili waweze kujiandikisha na kuondokana na maisha duni wanayoishi ndani ya Hifadhi.

Amesema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea na uhamasishaji wa wananchi ambapo kwa sasa  mwamko wa watu wanaoishi ndani ya hifadhi kutaka kuondoka umeongezeka huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuheshimu haki zote za msingi za wananchi hao.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa  Mamlaka hiyo Bw. Fedes Mdala ambaye pia  ni Meneja wa mradi huo amesema kuwa  hadi kufikia sasa  jumla ya kaya 934 zenye watu 5,747 na mifugo 26,227 zimeshaondoka ndani ya hifadhi.

 

Bw.Mdalla amesema hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo zimeendelea  kuchukuliwa na kuzitaja hatua hizo kuwa ni ujenzi wa nyumba, uhamasishaji, Uandikishaji wa maendeleo yaliyofanywa ndani ya Hifadhi na uhamishaji wa wanachi kwenda Msomera na maeneo mengine.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka wizara ya Mailiasili na Utalii Bw. John Mapepele amewapongeza wananchi hao kwa kufanya uamuzi sahihi ambao unakwenda kubadilisha maisha yao.


Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wenzake walioamua kuhama kwa hiyari  Bw. Jackson Olokida Laizer ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuwaondoa ndani ya hifadhi ambapo walikuwa wakikabiliwa na hali ngumu za maisha hasa kutokana na kuzuiwa kushiriki katika shughuli za kilimo na maendeleo.

Serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utali,Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na wizara nyingine za kisekta zinaendelea na utekelezaji wa kuhamisha watu kutoka ndani ya Hifadhi ili kuboresha maisha ya wananchi na kulinda hifadhi hiyo yenye hadhi mahsusi duniani.




Post a Comment

0 Comments