HEADLINES

6/recent/ticker-posts

MSTAAFU JAKAYA KIKWETE AKABIDHI VIDONGE VYA VITAMINI A KWA WATOTO NCHINI

 


Na Andrew Chale,
DAR ES SALAAM.

RAIS Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Menejimenti chini  ya Shirika la Nutrition International (NI) la nchini Canada amekabidhi vidonge vya matone vya vitamin A, milioni 22 ambavyo vitasaidia kuongeza kinga ya mwili na kuimarisha afya ya macho kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano Nchini.

Tukio hilo limefanyika mapema leo Dar es Salaam, 13 Machi 2024 katika bohari kuu ya dawa (MSD), wakati wa makabidhiano rasmi ya vidonge hivyo vya Vitamini A, kati ya NI na Wizara ya Afya tukio lililoshuhudiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Watoa huduma za Afya ya Jamii, Wananchi na Mwakilishi wa Balozi wa Canada nchini.

Katika tukio, Mhe Jakaya Kikwete,  amesema;

“Shirika la NI imetoa vidonge matone ya vitamin A, milioni 22 zitakazotolewa kwa awamu mbili, yaani mwezi Juni na Desemba kwa watoto takribani Milioni 11 walio chini ya umri wa miaka 5. 

Faida ya vitamin hivi ni kuimarisha afya ya macho na kuongeza kinga ya mwili kwa mtoto hivyo ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha watoto wanapatiwa matone hayo.” amesema Mhe. Jakaya Kikwete.

Aidha, Mhe Jakaya Kikwete amesema Shirika la NI, linatoa vidonge zaidi ya milioni 500 duniani kote kila mwaka na Tanzania hupata vidonge milioni 22.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel  amesema elimu ya mtoto inaanza siku mimba inatunga na sio shuleni kwa kumpatia Mama lishe iliyobora wakati wa ujauzito ili kusaidia kuimarisha ubongo wa Mtoto

“Wazazi zingatieni lishe bora kwa watoto tangu wa utangaji wa mimba na kuwa na desturi ya kula mlo bora kwa mama wajawazito na hii itamsaidia mtoto hata baada ya kuzaliwa na wakati yuko shule ubongo na akili yake kufanya kazi kikamilifu pia itamuepunga na magonjwa ya mara kwa mara” Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amewataka watanzania kuzingatia milo yao ya kila siku kwa kupata chakula chenye lishe hasa vyenye vitamini ili kuepugana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu , magonjwa ya moyo na kisukari

“Hivi sasa watu wanakula kupitiliza na hawazingati chakula nyenye lishe ivyo na kupelekea watanzania kusumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza kama uzito uliopitiliza, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kisukari. Niwatake wahudumu wa afya ngazi ya  jamii mkawape elimu watanzania waweze kutofautisha kati ya shibe na lishe” Amesema Dkt. Mollel.

Ameongeza kuwa awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha Tsh. bilioni 99 kwa ajili ya kuajiri na posho za wahudumu wa afya ngazi ya jamii pia wamekuwa msaada mkubwa wa kufikisha elimu ya lishe na afya bora kwa jamii

Nae Mwakilishi wa Balozi wa Canada, Helen Fytche amesema mwaka 2020 zaidi ya watoto milioni 100 duniani  walikosa vitamini A kutokana na Uviko-19 na ili kusaidia nchi 16 mwaka 2021 walitoa dozi 124 zilizosaidia kuzuia vifo 32 milioni.

Amesema uongezaji wa vitamini A huimarisha mfumo wa kinga kwa watoto chini ya miaka mitano na kuepusha vifo vinavyoweza kuepukika na kinga magonjwa ya kawaida ikiwamo surua na kuharisha.

Amesema wanaiunga mkono Serikali katika kutekeleza sera na miongozo ya kimataifa na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa kuwa kwa sasa chanjo ya kitaifa imezidi asilimia 98 ijapokuwa kwa mwaka 2020 ilishuka kutokana na Uviko-19.

Hata hivyo, Mkurungenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga amesema Tanzania ilianza kutoa huduma ya matone ya vitamini A miaka 37 iliyopita.

Amesema  wakati wote wamehakikisha huduma inatolewa kwa watoto kuwafanya wawe na kinga imara ya mwili na kuimarisha uwezo wa macho kuona.

Mbali ya Vitamini A, wamekuwa wakitoa elimu kwa kinamama kuwaongezea vyakula mbalimbali kama mbogamboga, mafuta ya mawese, nyama kama maini na karoti ili kuimarisha vitamini hiyo.

"Takwimu zinaonyesha asilimia 44 ya watoto chini ya miaka mitano wana changamoto ya ukosefu wa vitamini A kutoka kwenye milo, ndiyo maana tunatoa kwa watoto wa miezi sita  mpaka 56 yaani miaka mitano.

"Kila baada ya miezi sita tunatoa Juni na Desemba siku zote 31 za mwezi na tunawafikia watoto milioni 10, mwaka huu tunalenga kuwapata milioni 11 kwa dozi zote mbili," amesema.


 

Post a Comment

0 Comments