HEADLINES

6/recent/ticker-posts

UPASUAJI WA MGONGO KWA NJIA YA MATUNDU WAFANYIKA KWA MARA YA KWANZA NCHINI


Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imefungua kurasa mpya katika matibabu ya kibingwa na kibobezi hapa nchini ambapo kwa mara ya kwanza imeanzisha huduma ya upasuaji wa mishipa ya mgongo kwa njia ya matundu kitaalam (Endoscopic neurospine surgery).

Huduma hiyo imekuja kufuatia matokeo ya kongamano  la Kimataifa la madaktari bingwa wa ubongo na mgongo na mishipa ya fahamu (Global Neurosurgery course) lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya MOI na Chuo kikuu cha Weill Cornell cha Marekani na wataalam 120 wanashiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI Prof. Abel Makubi amesema tayari wagonjwa 13 wa mgongo wamefanyiwa upasuaji kwa mafanikio makubwa katika siku mbili (Jumatano na Alhamisi) toka kuanza kwa huduma hiyo.

Prof.Makubi amesema kwa huduma hiyo iliyoanzishwa Hospitalini hapo itasaidia kupunguza adha na gharama kubwa za kufata matibabu nje ya nchi kwa sababu itakua inapatikana hapa nchini.

“Hii ni kwa mara ya kwanza kwa MOI na ni mara ya kwanza kwa Taifa kufanya upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu (Endoscopic Spine Surgery), kwa dhati tunakishukuru chuo kikuu cha Weill Cornel cha Marekani kwa ushirikiano huu muhimu na kwa niaba ya menejimenti naahidi tutauenzi” amesema Prof. Makubi 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Mgongo kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornel Marekani Prof. Roger Hartl ameahidi kuendeleza ushirikiano na Taasisi ya MOI katika kuendelea kuwajengea uwezo wataalam, kuwezesha tafiti za kisayansi na vifaa tiba vya upasuaji ili iweze kuwa kituo mahiri cha upasaji wa mgongo barani Afrika.

“Lengo letu kuiona MOI ikiwa kituo cha umahiri kwenye kutoa tiba na mafunzo kwa mataifa mengine juu ya upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu, nimefurahi kuona namna ambavyo MOI inathamini ushirikiano wetu na ninaahidi kuuendeleza” amesema Prof. Hartl

Post a Comment

0 Comments