HEADLINES

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA SAUDI ARABIA TANZANIA


Na Mwandishi Wetu,

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax Mei 14, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Balozi Yahya Bin Ahmed Okeish katika Ofisi ndogo za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Jijini Dar es Salaam. 

Balozi Yahya Bin Ahmed Okeish alimueleza Waziri wa Ulinzi na JKT utayari wa Falme ya Saudi Arabia kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yanayohusiana na Wizara ya Ulinzi na nchi kwa ujumla. Balozi Ahmed alisema Tanzania ni nchi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo Falme ya Saudi Arabia ingependa kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za Kiuchumi, Utamaduni na Kijamii na ingependa kuendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo ya muda mrefu. 

Nae Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alimshukuru Balozi Yahya Bin Ahmed kwa kufika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya kuendeleza uhusiano wa kindugu na wa muda mrefu baina ya Tanzania na Saudi Arabia. Waziri wa Ulinzi Dkt. Stergomena Tax alimuhakikishia Balozi Ahmed kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano uliopo wa nchi hizo mbili. 

Aidha, Waziri Tax amemwambia Balozi Ahmed utayari wa Wizara ya Ulinzi na JKT kushirikiana na Ufalme wa Saudi Arabia katika masuala ya Ushirikiano wa Kijeshi, Mafunzo na kubadilishana utaalamu na kukabiliana na changamoto za kiusalama za ugaidi na uhalifu wa mtandaoni. 

Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa waliokuwa na Waziri wa Ulinzi na JKT katika mazungumzo hayo ni pamoja na Kamishna wa Utafiti na Maendeleo Jeshini, Rear Admiral Michael Mumanga na Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa ya Kijeshi, Kanali Singano Wibonela.


Post a Comment

0 Comments